HISTORIA YA KUTUNGA KATIBA NA USHIRIKI WA VYAMA VYA SIASA TANZANIA. (SEHEMU YA PILI)

TANU wakati huo ilifutilia mbali shirikisho la vyama vya wafanyakazi lililoitwa Tanganyika Federation of Labour (TFL) kwa kutunga sheria mpya National Union of Tanganyika Workers (Establishment) Act 1964. 

Sheria hii pia ilianzisha shirikisho jipya la wafanyakazi. Athari bayana ya sheria hii ni pamoja na kuua uhuru wa vyama vya wafanyakazi nchini; na vyama vya wafanyakazi vilianza kuwekwa chini ya chama tawala na kufanya matawi ya TANU.

Hili lilifuatiwa na kufutwa kwa vyama vya siasa vya upinzani mwaka 1965 na kuanzisha mfumo wa siasa wa chama kimoja. 

Hapa katiba ya mwaka 1965 Ibara ya 3 ilitamka kuwa Tanzania ni nchi inayofuata mfumo wa chama kimoja na kuanisha kuwa TANU ndicho chama pekee kisheria Tanzania Bara na Afro-Shiraz Party (ASP) kiliendelea kuwa chama pekee huko Zanzibar. 


Hii ni kufuatia muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoundwa tarehe 26 Aprili 1964. Zaidi sana matakwa ya mfumo wa chama kimoja yalianisha kuwa masuala yote ya siasa mbali na yaliyohusu mihimili ya dola yaani bunge, mahakama na serikali yalifanywa chini ya chama tawala au moja kwa moja na chama chenyewe. 

Kilele cha  TANU kilifikiwa mwaka 1975 pale chama kiliposhika hatamu yaani chama kuwa ndicho chenye sauti na maamuzi ya mwisho katika kila jambo nchini. 

Hapa serikali na mihimili yake ya dola ilitiwa mfukoni mwa chama tawala. Ilikuwa vigumu kutenganisha chama na serikali. Huo ulikuwa ndiyo mwanzo wa “chama dola” cha (Shivji 2006)

Ingawa matukio yaliyotajwa hapo juu yaliashiria kuwepo mfumo wa chama kimoja kisheria, wanazuoni wengi wanakubaliana kuwa mfumo huo ulikuwepo tangu mwanzoni mwa miaka ya 1962 (Baregu 1995; Makulilo 2008; Mukandala 2002; Ahluwalia na Zegeye 2001). 



  Ifahamike kuwa chama tawala ndicho kilihusika moja kwa moja kutunga katiba kwaniaba ya wananchi. Serikali ilikuwa ikitekeleza tu maagizo ya chama. Pili wananchi walipokonywa haki yao ya kuhusika kutunga katiba mpya na hivyo katiba kutafsiriwa kama “mkataba kati ya watawala na watawaliwa” kinyume cha tafsiri ya sasa kuwa “katiba ni mwafaka wa kitaifa.” 

 

Kuelekea mageuzi ya mfumo wa kisiasa toka chama kimoja kwenda demokrasia ya vyama vingi, suala la katiba mpya lilipendekezwa na tume ya Rais.

Hata hivyo CCM ilipuuza mapendekezo ya kutunga katiba mpya. Licha ya utetezi mbalimbali kutolewa na chama tawala na serikali yake kukataa kutunga katiba mpya, ukweli unabaki kuwa hofu ya CCM kung’olewa madarakani imeendelea kuwa tatizo. 


Waasisi wa CCM wanadai kuwa ili hoja ya katiba mpya iweze kuwa na mantiki ni lazima walau jambo moja litokee kati ya haya: mabadiliko ya dola; kuunganika kwa dola; katiba iliyokuwepo kufutwa na dikteta; pale demokrasia inapoangusha utawala wa kibaguzi; na yanapotokea mazingira maalum (Msekwa 2000).


Baadhi ya Wana CCM wamekuwa wakidai kuwa kuhitajika kwa katiba zilizopita kulitokana na kuwepo kwa walau moja ya mazingira hayo. Na kuwa kubadili mfumo wa siasa toka chama kimoja kwenda vyama vingi pekee haijitoshelezi kuwa hoja ya katiba mpya kama ilivyopendekezwa na tume ya Rais ya mwaka 1991. Inaendele sehemu ya Tatu



 

Comments

Popular posts from this blog