KUSITISHWA KWA 'AFRIKANAIZESHENI' KULISABABISHA KUASI KWA JESHI LA TANGANYIKA MWAKA 1964

SEHEMU YA PILI

KAWAWA 'SIMBA WA VITA' JEMBE LA AFRIKANAIZESHENI

Ili kuepusha shari, na ili Chama kisifarakane, Mwalimu akajiuzulu nafasi yake ya Uwaziri Mkuu wa Tanganyika Januari 16, 1962 ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu Uhuru wa nchi mpya, na kuamua kurejea kijijini kuimarisha Chama kama Mwenyekiti wa Taifa wa TANU; na Rashid Kawawa akachukua nafasi ya Uwaziri Mkuu. Naye Oscar Kambona, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Elimu, akawa Waziri wa Mambo ya Ndani badala ya Clement George Kahama. Wote wawili hao, Kawawa na Kambona wakaachiwa kazi ya kuwaondoa Wazungu katika vyeo walivyokuwa bado wanashikilia haraka bila visingizio.

Akimteua Kawawa, Mwalimu alisema kwa hasira na kwa kuamrisha: “Tazama, Rashid, wewe ndiye Waziri Mkuu kuanzia sasa hivi. Shika kiti”. Na akijulisha mawaziri wake juu ya uamuzi huo, Mwalimu alisema: “Leo naacha kiti changu cha Waziri Mkuu. Kabla ya kujiuzulu, mimi mwenyewe nimechagua upya Baraza la Mawaziri, na Bwana Kawawa akiwa ndiye Waziri Mkuu na ninyi wengine wote mtabakia katika Baraza la Mawaziri”.

Kujiuzulu kwa Mwalimu Nyerere kulitoa nafasi kwa zoezi la kuwaondoa na kutimua kazini wazungu na wageni wengine wasio Waafrika kwa kasi ya kutisha, na nafasi zao kujazwa na Watanganyika weusi, maarufu kama “Africanisation” – Afrikanaizesheni, zoezi ambalo mapema, Mwalimu alisema kuwa ni ubaguzi mbaya kuliko wa makaburu. Kawawa na Kambona walipewa jukumu hili kama wanaume wa shoka wasiosikia la mtu. 

Kazi ya kwanza ya Kambona ilikuwa ni kumtimua Kamishna wa Polisi Mwingereza, na kumteua Komredi Elangwa Shaidi kuchukua nafasi hiyo, Elangwa Shaidi alikuwa ni Mpare kutoka Jimbo la Tanga, lakini uteuzi huo wa Kambona bado haukuwaridhisha wengi kwa kuwa hakufanya mabadiliko kwa Jeshi (T. R.). Zoezi hili la “Africanisation” lilifanywa kwa kasi ya kutisha kiasi cha kuishitua jamii ya Kimataifa. 

Kufikia mwishoni mwaka 1962, nusu ya kazi za vyeo vya juu na vya kati serikalini ukiondoa Jeshi, zilikuwa zimeshikwa na Waafrika, wengi wao wasio na ujuzi wa kutosha kuweza kuzimudu.

Lakini kwa dhahiri ilionekana kuwa Mwalimu Nyerere alikwenda kujipanga ili kuja na mbinu mpya za kuwadhibiti maadui zake, kwa dhahiri ilionekana Mwalimu hakupenda nafasi za juu katika Jeshi la Tanganyika, T.R, zishikwe na Watanganyika weusi kwa kuwa hofu ya kupinduliwa ilikuwa juu sana, hasa kwa kuwa wakati huo matukio ya namna hiyo yalishaanza kujitokeza katika nchi mbalimbali za Kiafrika zilizokuwa na Wakuu wa Majeshi Waafrika.

Chini ya Kawawa kama Waziri Mkuu, mabadiliko mengi yalifanyika, yakiwamo kufutwa kwa sheria ya kumiliki ardhi kwa maana ya mtu kupewa kabisa ardhi yote, na kuwa ardhi kwa kukodishwa. Pia Bunge lilipitisha Katiba kufanya Tanganyika kuwa Jamhuri chini ya Rais Mtendaji badala ya Gavana Mkuu aliyemwakilisha Malkia,hatua iliyoelezewa kuwa ya kuleta “chemchem mpya ya utii na kuwatia moyo wananchi wakaipende nchi yao”.

Pia ilipitishwa sheria ya kumpa Rais uwezo wa kumtia mtu kizuizini bila kutoa sababu, pamoja na kupiga marufuku migomo ya wafanyakazi. Kwa hatua hizi, gazeti la “London Express” lilipiga kelele kuwa “aina ya udikteta unaingia Tanganyika”, kwa njia ya mamlaka makubwa anayopewa Rais chini ya Katiba ya Jamhuri”.

 





 

Comments

Popular posts from this blog