MKUTANO WA WADAU WA DEMOKRASIA KUJADILI MASUALA MAHSUSI YA ZANZIBAR


Demokrasia ni nini?
Demokrasia ni mfumo wa serikali ambapo wananchi wote ni sawa mbele ya sheria na wanashiriki katika kufanya maamuzi ya kitaifa juu ya masuala ya Umma. Wakati mwingine wananchi hushiriki moja kwa moja - hii ina maana kwamba wao hupiga kura moja kwa moja kwenye masuala kama vile sheria na katika chaguzi. Wakati mwingine huwakilishwa na viongozi wao waliowachagua. Ni utawala wa watu, na watawala hutawala kwa ridhaa ya watu.
Kwa hiyo kwa kifupi Demokrasia ni mfumo unatoa fursa ya madaraka kwa Umma moja kwa moja au kutokana na uwakilishi.
Abraham Lincoln, Rais wa 16 wa Marekani, alisema Demokrasia ni serikali ya watu/mfumo wa utawala wa watu, kwa ajili ya watu na unaotokana na watu. Watu wanaunda serikali.

Aina za demokrasia
1. Demokrasia ya moja kwa moja (kwa Kiingereza "Direct Democracy") ni aina ya demokrasia ambayo wananchi wote wanaweza kushiriki katika kuamua masuala ya kisiasa, ya kijamii, ya kisheria na ya kiuchumi bila kutumia chombo cha uwakilishi kama vile bunge. Uwezo huu wa wananchi kutoa maamuzi unaweza kuwapa hata uwezo wa kimahakama, ingawa mara nyingi wananchi hupewa uwezo wa kutunga au kupitisha sheria tu.
Demokrasia ya moja kwa moja ni tofauti na demokrasia inayofuatwa katika nchi nyingi duniani hivi sasa, ambapo wananchi huchagua wawakilishi wao katika uchaguzi. Nchi ya Uswisi ni maarufu kwa mfumo wake wa demokrasia ya moja kwa moja ambako sheria nyingi zinaamuliwa na wananchi wote kwa njia ya kura.
2. Demokrasia shirikishi ("Representative Democracy"): hapo wachache hupewa na wengi dhamana katika uwakilishi wa jamii katika maamuzi. Wachache huchaguliwa na wengi kwa njia ya demokrasia huru na ya haki kwa kufuata Katiba ya nchi hiyo. Mfano: Wabunge huwakilisha wananchi wao katika kuleta maendeleo na kuishauri serikali juu ya maendeleo ya nchi yao.
Misingi ya demokrasia
·       Uwepo wa vipindi vya uchaguzi wa viongozi na chaguzi zenye kuzingatia haki na usawa.
·       Kuwepo uchaguzi huru na uwanja sawa wa kisiasa.
·       Wananchi wawe na fursa kikatiba kupata taarifa, vyanzo vya taarifa viwepo na kulindwa kisheria.
·       Wananchi na wanajamii wawe na fursa ya kuunda vyombo vya kijamii mathalani asasi za kiraia.
·       Kuwa na taasisi zinazolinda na kuchochea ustawi wa demokrasia nchini.
Umuhimu wa demokrasia
·       Kukosoa matumizi mabaya ya fedha na viongozi kwa misingi ya demokrasia.
·       Kushirikishwa kupanga kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
·       Kuunga mkono jitihada za serikali katika kuchochea ustawi na maendeleo kwa jamii.
·       Kuhoji utendaji wa serikali kuanzia ngazi ya mtaa, kata, kijiji, wilaya kuhakikisha uwazi, uadilifu na uwajibikaji.
Faida za demokrasia
·       Matumizi mazuri ya rasilimali za nchi.
·       Maendeleo endelevu.
·       Kupungua kwa umasikini, ujinga na maradhi.
·       Kutokomea kwa rushwa.
·       Huduma bora za jamii.
·       Amani na utulivu.
·       Kuheshimiwa kwa haki za binadamu.
·       Utatuzi wa migogoro kwa mujibu wa sheria na taratibu.
·       Kuleta ustawi wa wananchi.
 
 

 

Comments

Popular posts from this blog