ISEMAVYO SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA,2017
- “Mtu anayesaidiwa” maana yake ni mtu anayepatiwa msaada wa kisheria chini ya sheria hii.
- “Mtu asiye na uwezo” Maana yake mtu asiye na uwezo wa kumudu gharama za wakili wa kujitegemea ikiwa ni pamoja na makundi mengine ya watu kama itakavyohitajika kwa maslahi ya utoaji haki.
- “Ushauri wa Msaada wa kisheria” Maana yake ni ushauri na msaada unaotolewa kwa mtu asiye na uwezo katika mashauri ya jinai na madai kuhusu sheria husika, taratibu za kisheria na uandaaji wa nyaraka za kisheria.
- “Msaada wa kisheiria” au “huduma ya msaada wa kisheria”inajumuisha utoaji wa ushauri wa kisheria, usaidizi wa kisheria au uwakilishi kwa watu wasiokuwa na uwezo.
- “Mtoa huduma wa msaada wa kisheria” Maana yake ni taasisi iliyosajiliwa chini ya sheria hii kutoa huduma ya msaada wa kisheria.
Sheria hii imeanzisha vyombo viwili vya uratibu.
(a) Bodi ya Taifa ya Ushauri ya Msaada wa kisheria ambayo inaundwa na wajumbe wafuatao kwa kuzingatia uwakilishi wa kijinsia. Muda wa kukaa madarakani kwa wajumbe wa bodi itakuwa miaka mitatu lakini wanaweza kuteuliwa tena kwa kipindi kingine cha miaka mitatu tu.
o Mwenyekiti ambaye ni Jaji wa mahakama kuu ya Tanzania atakayeteuliwa na waziri husika akisaidiana na Jaji Mkuu
o Mwanasheria Mkuu au mwakilishi wake mwenye cheo si cha chini ya Afisa Sheria
o Mwakilishi mmoja kutoka jukwaa la taifa la haki jinai
o Mwakilishi mmoja kutoka Chama cha Mawakili wa kujitegemea Tanganyika
o Mkurugenzi wa huduma za sheria kutoka wizara inayohusika na tawala za mikoa na serikali za mitaa au mwakilishi wake
o Mwakilishi wa watu wanaoishi na ulemavu
o Mwakilishi mmoja kutoka taasisi zinazowakilishi wasaidizi wa kisheria
o Katibu wa Bodi ya taifa ya ushauri wa msaada wa sheria atakuwa ni msajili
Miongoni mwa majukumu ya bodi,Kutoa miongozo ya kisera, kutoa ushauri, Kupitisha ripoti za mwaka za watoa huduma ya msaada wa sheria na kupokea na kutoa maamuzi ya rufani zitakazo pitia maamuzi ya msajili wa watoa huduma za msaada wakisheria.
(b) Ofisi ya msajili wa watoa huduma wa msaada wa kisheria.
(c) Katika ngazi ya taifa kutakuwa na msajili na katika ngazi ya wilaya na mkoa kutakuwa na wasajili wasaidizi. Miongoni mwa kazi zao itakuwa ni pamoja na; Kusajili watoa huduma wa msaada wa kisheria, Kuchunguza malalamiko yote yanayohusiana na watoa huduma ya msaada wa kisheria, Kusimamisha au kufuta usajili wa mtoa huduma ya msaada wa kisheria,kutunza kumbukumbu ya orodha ya watoa huduma ya msaada wa kisheria, Kukagua ofisi za watoa huduma ya msaada wa kisheria ikiwa ni pamoja na kujiridhisha na aina na ubora wa huduma zitolewazo, kutoa elimu ya sheria na ufahamu miongoni mwa wanajamii,aidha, wataratibu na kuwezesha utayarishaji wa mitaala ya kufundishia wasaidizi wa kisheria kwa kushirikisha wadau muhimu.
Comments
Post a Comment